Showing posts with label siasa za bongo. Show all posts
Showing posts with label siasa za bongo. Show all posts

CHADEMA YAMWAGA NYARAKA ZA SIRI KUMJIBU ZITTO KABWE...YAWATAKA MSAJILI WA VYAMA NA CAG WAWAJIBIKE, ZICHEKI HAPA

Hii ni taarifa  ya  Chadema:
Kutokana na taarifa zilizotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya hesabu za Serikali kuwa vyama vya siasa ambavyo vinapata ruzuku kutoka serikalini havijawasilisha taarifa yake ya mapato na matumizi kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kipindi cha miaka minne mfululizo, yaani kuanzia mwaka 2009/2010- 2012/2013.

CHADEMA tunapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo juu ya taarifa hizo;
     i.  Kuwa taarifa hizo sio sahihi na hazina ukweli kuhusiana na CHADEMA labda kwa vyama vingine, hii ni kutokana na ukweli kuwa tulishawasilisha taarifa zetu za fedha kwa msajili wa vyama vya siasa na zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha 2010/2011, 2011/2012 na hili linathibitishwa na barua ya msajili wa vyama vya siasa yenye Kumb.Na. CDA.112/123/01a/37, ya tarehe 04 september 2012. Iliyopelekwa kwa makatibu wakuu wa vyama vyote vya siasa (nakala imeambatanishwa).

Aidha, hesabu za mwaka wa fedha zilizokaguliwa za 2009/2010, tuliziwasilisha kwa Msajili wa vyama vya siasa kwa barua yenye Kumb.Na. C/HQ/ADM/MSJ/04/71 ya tarehe 27 Octoba, 2011. (Nakala ya barua imeambatanishwa)

    ii. Kuhusu taarifa ya fedha iliyokaguliwa kwa mwaka huu wa fedha 2012/2013, bado haijawasilishwa kwenye ofisi za msajili wa vyama kutokana na barua ya msajili wa vyama vya siasa ya Novemba 26, 2012 yenye Kumb.Na.DA.112/123/16A/97 ambayo ilikuwa na maelekezo kuhusu ukaguzi wa mahesabu ya vyama vya siasa, iliyokuwa inajibu barua tuliyomwandikia tukitaka kupata ufafanuzi kuhusu ukaguzi wa hesabu za chama kutakiwa kufanywa na CAG na alitujibu kuwa “tumefanya mawasiliano na Mkaguzi na Mdhibiti wa Mahesabu ya Serikali (CAG) kwa ufafanuzi wa jambo hili na tutawafahamisha ipasavyo kuhusu malipo/gharama mliyotakiwa kulipa katika ukaguzi wa Mahesabu hayo”; mpaka leo hatujawahi kupata ufafanuzi huo pamoja na ukweli kuwa tumeshafunga hesabu zetu za mwaka kama chama (barua imeambatanishwa).

    iii. Kuhusu taarifa ya fedha kutoka nje ya nchi, CHADEMA tumekuwa tukiwasilisha taarifa zetu kila mara tunapopata fedha kwa ajili ya mafunzo na programu nyingine mbalimbali za chama kama ambavyo msajili alituandikia barua tarehe 19 Agosti 2013 yenye Kumb. Na.DA.112/123/16a/10 iliyokuwa ni taarifa ya mapato yatokanayo na michango au misaada toka nje ya nchi, alisema “tunashukuru kwa taarifa hii ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya vyama vya siasa” (imeambatanishwa barua husika )

   iv.Kuhusu Taarifa za gharama za uchaguzi kwa mwaka 2010 , tuliwasilisha taarifa hiyo na Msajili alikiri kuwa ni vyama viwili tu ndiyo vilikidhi utekelezaji wa sheria ya gharama za uchaguzi kwa ukaguzi wa marejesho, hii inathibitishwa na barua ya Msajili yenye Kumb.Na. CDB.173/205/01/23 ya tarehe 16 April, 2012. (Nakala imeambatanishwa)

     Tunapenda kuwahakikishia watanzania kuwa CHADEMA ndiyo ambayo tulidai CAG awe na mamlaka ya kukagua fedha za vyama vya siasa ili taarifa zake ziwekwe hadharani na tutaendelea kutoa ushirikiano kama ambavyo tumekuwa tukifanya siku zote, kuhakikisha sheria hii inatekelezwa ipasavyo kuhakikisha uwazi kwenye mapato na matumizi ya vyama vya siasa.

Aidha, kama ambavyo siku zote tumesimamia na kusisitiza, tunamtaka CAG akague fedha zote za vyama na sio ruzuku tu kama ambavyo kamati ya Bunge inataka iwe.

Imetolewa leo Alhamis, Oktoba 17, 2013;
……………………….
Antony C. Komu
Katibu wa Baraza la Wadhamini.


HUYU NDO KIONGOZI ALIYEFUNGUKA NA KUSEMA KUA NYERERE ANGEKUA HAI, ANGESHAHAMIA CHADEMA. SOMA HAPA

Aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Tanzania (BoT) na baadaye mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei ameeleza jinsi alivyokuwa karibu na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere hadi kupata kazi hiyo ya juu.
Zaidi, kwenye mahojiano maalumu, nyumbani kwake Tengeru, Arusha, Mtei anabashiri kuwa iwapo kiongozi huyo angekuwa hai hadi leo, bila shaka angeachama na chama chake alichokiasisi na kujiunga na Chadema. Endelea…
Swali: Umepata kufanya kazi na Mwalimu Julius Nyerere, hivi huyu alikuwa ni mtu wa aina gani?
Jibu: Nilimfahamu Mwalimu mwaka 1959 mwishoni niliporudi nyumbani nikitokea masomoni Makerere nchini Uganda. Unajua Serikali ya Kikoloni haikunipa kazi, nikaamua kwenda Kenya kufanya kazi.
Siku moja nilikwenda kumtembelea Mwalimu nyumbani kwake nikiwa na rafiki yangu Mwanjisi, Mwanjisi ndiye aliyenipeleka.

Tulikaa tukaongea na tukafahamiana, ndipo alipotuambia kwamba ipo siku wakoloni wataondoka na sisi tutalitumikia taifa letu.
Mwalimu alikuwa ni mtu jasiri, ndiye aliyethubutu kuwaambia wakoloni waondoke, lakini hapo awali watu walikuwa wakiogopa kusema.

Yeye alisimama na kukemea ubaguzi wa aina yoyote.
Mwalimu pia alipenda haki na usawa. Hakupenda kabisa uonevu, lakini tatizo lake alikuwa haambiliki. Kile alichokisema alitaka hicho hicho kifuatwe, hakupenda mtu wa kumwambia hapana.
Swali: Mwalimu Nyerere alichukia nini enzi za uhai wake?
Jibu: Alichukia wezi wa mali ya umma na yeyote yule aliyekuwa mdokozi alimfukuza mara moja bila kumwonea haya. Unajua, Mwalimu alipobaini kwamba kuna mtu katika idara fulani hata wizara ni mzembe au mvivu, alimhamishia sehemu nyingine.
Mwalimu alikuwa tayari kuhakikisha wananchi wanamiliki rasilimali zao kama madini na wanazifaidi na siyo kuwapa wageni. Yeye alipenda Watanzania wafaidi rasilimali zao siyo chini ya asilimia hamsini.
Alisema wazi kabisa kwamba haya madini yaliletwa na Mungu hayakujileta yenyewe, hivyo alipenda wazawa wazifaidi rasilimali zao na siyo wageni.
Mimi nashangaa, baadhi ya viongozi wa CCM wa sasa tofauti na Nyerere, hawalioni hilo. Kuna tofauti kubwa kati yao na Mwalimu. Yeye aliwapenda watu wake lakini viongozi wa CCM wanawachukia watu wao na kuwakumbatia wageni wanaowaita wawekezaji.

Swali: Ni tukio gani ambalo huwezi kulisahau wakati ukifanya kazi na Mwalimu Nyerere?
Jibu: Siwezi kusahau kipindi ambacho nilijiuzulu ugavana kwani tulitofautiana sana na Mwalimu hadi nikaamua kuuza nyumba yangu Dar es Salaam na kuhamia Arusha, na hapa nimekuwa mkulima hadi leo.
Unajua Mwalimu alikuwa mtu asiyependa demokrasia hata kidogo, alikuwa mtu ambaye haambiliki, yeye alipenda kile alichokisema tu kitekelezwe.
Mwaka 1977 Mwalimu Nyerere walitofautiana na Mzee Kenyata na alifunga mpaka wa Tanzania na Kenya, wakati huo Milton Obote (Rais wa Uganda enzi hizo) alikuwa ameporwa madaraka na Idd Amin na ndipo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikavurugika.
Mimi nikiwa ni Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo niliamua kurudi nyumbani.
Niliporudi nikapewa nafasi ya kuwa Waziri wa kwanza wa Fedha, wakati huo tukiwa katika vita ya Uganda na mimi ndiye nilikuwa nikisimamia masuala ya uchumi na fedha wakati wote wa vita. Vita ilipoisha nchi yetu iliingia katika mtikisiko mkubwa wa kiuchumi, hatukuwa na fedha kabisa.
Ndipo nikaamua kumshauri Mwalimu, kwamba tukope fedha katika Benki ya Dunia ili kutatua suala hili. Baada ya kushauriana na watu wa Benki ya Dunia nilimwambia Mwalimu pia tupunguze bajeti ya matumizi yetu, nilimshauri vitu vingi kwa kweli.
Unajua, Mwalimu alinijibu kwamba mimi nimeshawishiwa na watu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), ndipo nikaamua kujiuzulu. Huwezi kuamini na siku najizulu Mwalimu alitoa hotuba ya kuridhia kujiuzulu kwangu na kusema kwamba ‘kamwe hawezi kuruhusu serikali yake iongozwe kutoka Washington.’
Hakika nilishtushwa na hotuba yake baada ya mimi kujiuzulu ukizingatia ya kwamba mimi nilikuwa nimelitumikia taifa langu kwa uadilifu mkubwa, ndipo nikaamua kuwa mkulima hadi leo. Niliuza nyumba yangu Dar es Salaam na kununua shamba kubwa hapa Tengeru mkoani Arusha.
Mwalimu alipenda watu wa kumwambia ‘ndiyo mzee’ na bahati mbaya mimi sikuwa mtu wa namna hiyo. Kila alichokisema alitaka kifuatwe na hata umma unajua kwamba mimi nilithubutu kumwambia Mwalimu ‘hapana’

Swali: Ni jambo gani zuri ambalo unalikumbuka kwa Mwalimu Nyerere?
Jibu: Kwanza kabisa, yeye ndiye mwasisi wa taifa letu, alipenda sana nchi yake na hata pia alipenda uhuru wa nchi nyingine barani Afrika. Ndiyo maana wakati mwingine alikuwa tayari kuchelewesha uhuru wa Tanganyika ili nchi nyingine za Afrika zipate uhuru.
Hakika, Mwalimu aliipenda sana Afrika, alisaidia harakati za ukombozi wa nchi mbalimbali za Afrika, alikuwa mzalendo wa kweli ambaye hakuwahi kutokea kabisa kabla yake.
Hii nchi aliyoipigania Mwalimu ibaki moja, tusiigawe vipande vipande. Isiwe kundi la watu fulani linapokea mapesa na wengine wanyonge wanataabika, wanakufa na njaa. Leo tunasikia kuna vigogo wanaficha mapesa nje ya nchi hii ni ajabu sana”.

Swali: Iwapo Mwalimu Nyerere angelikuwa hai, je, unadhani angekemea mambo gani?
Jibu: Kwanza kabla ya kukujibu, Mwalimu angekuwa hai leo nakuambia kwanza tayari angekuwa ameshajiunga Chadema.

Na tuna imani huko aliko anatupigia makofi kwa kazi nzuri tunayoifanya ya kukemea ufisadi na rushwa kama sera yake ilivyokuwa.
Unajua Mwalimu enzi za uhai wake alishawahi kutuambia mbele yangu kwamba Chadema ndicho chama mbadala wa CCM.

Ndicho chama kitakachoweza kuongoza nchi hii baada ya CCM na leo tunaona utabiri wake. Lakini, niseme angekuwa hai angekemea vitendo vya kukithiri kwa rushwa na ufisadi, kwani sasa tunaona kundi la walionacho na wasionacho linavyokua hapa nchini.
Swali: Je, unadhani misingi aliyoiacha Mwalimu Nyerere inafuatwa leo hii?
Jibu: Kwanza kwa uhuru aliotupatia, hilo hakuna mtu wa kutupora. Kingine, misingi yake haifuatwi kabisa.

Mwalimu alipenda haki na usawa, maskini wapate na matajiri wapate, lakini kwa hali ya sasa hatuna viongozi wa kukemea rushwa wala ufisadi kwa kuwa hata wao wamechaguliwa kutokana na mkondo wa rushwa. hiyo hiyo.

ZITTO KABWE ATIMIZA AHADI YAKE,ATAJA MSHAHARA WA RAIS KIKWETE.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania analipwa sh milioni 384 kwa mwaka, sawa na sh milioni 32 kwa mwezi pasipo kukatwa kodi.
Hii ni mara ya pili kwa Zitto kutangaza hadharani mishahara ya viongozi wakuu wa serikali, akiwa ameanza na ule wa Waziri Mkuu, aliyesema analipwa takribani sh milioni 26 kwa mwezi.
  
Akiwahutubia wananchi mjini Igunga jana, ukiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha chama Kanda ya Magharibi, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini alisema kuwa sababu ya kutaka mishahara ya viongozi wakuu wa nchi ijulikane, ni kuzuia mianya ya watu wachache kuiibia nchi kutokana na usiri wa jambo hilo.
  
Zitto alisema hoja ya msingi si kiasi wanacholipwa viongozi hao walioajiriwa na wananchi, bali ni usiri unaofanywa juu ya kiwango hicho jambo alilosema kuwa linaweza kutumiwa na wajanja kuendelea kuinyonya nchi.
  
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona mwalimu anayelipwa mshahara wa sh 220,000 kwa mwezi akikatwa kodi, huku viongozi wa kuchaguliwa wakiwa wanapokea mishahara mikubwa pasipo kukatwa kodi licha ya kuhudumiwa kila kitu na serikali.
  
Aliongeza kuwa katiba ya sasa Ibara ya 43(1), inaeleza kuwa rais atalipwa mshahara pamoja na malipo mengine, huku ibara hiyo hiyo kifungu cha pili ikizuia mshahara na marupurupu kupunguzwa, hali aliyoelezea kuwa ni muhimu katiba mpya ikabadilisha sheria hizo kwa manufaa ya nchi.
  
“Kwa hiyo hata kesho kama Dk. Willibrod Slaa akiwa rais na akataka kupunguza mshahara wake, kwa katiba hii hawezi na hili jambo si sahihi kwani viongozi wa ngazi hizi wanapata kila kitu bure kutoka serikalini,” alisema Zitto.
  
Akiwa katika Kata ya Choma, Zitto alikagua kilichokuwa kiwanda cha kuchambulia pamba cha Giner ambacho kimeacha kufanya kazi tangu mwaka 1998.
  
Alisema kufa kwa viwanda vingi vya uzalishaji nchini kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, akidai kuwa alishindwa kutofautisha suala la uwekezaji na biashara huru.
  
“Ni serikali ya Mkapa ndiyo ilitufikisha hapa katika kupotea kwa viwanda nchini, wao walidhani biashara huru ni kuwapa wawekezaji viwanda vyetu na serikali kujiweka pembeni, sasa nchi imebaki kutegemea uchumi wa uchuuzi badala ya uzalishaji,” alisema.
  
Alisema sera ya uwekezaji katika Serikali ya CCM ilichukuliwa kama fursa ya viongozi wa chama hicho kujinufaisha na mali za serikali pasipo kujua wataendeleza vipi.
  
Zitto alisisitiza kuwa kila mara CHADEMA imekuwa ikisisitiza bungeni juu ya kupiga marufuku usafirishaji wa pamba kwenda nje kama malighafi, na badala yake wakitaka viwanda vifufuliwe kwa ajili ya kutoa ajira kwa Watanzania.
  
Alirejea kusisitiza sera ya hifadhi ya jamii kwa wakulima akisema imefikia wakati serikali kupitia SSRA ione umuhimu na ulazima wa kuhakikisha wanaongeza Watanzania wenye hifadhi ya jamii kwa kuanza mfumo maalumu wa hifadhi ya jamii kwa wakulima (Supplementary scheme for social security to small holder farmers).
  
“Ninapendekeza serikali ichangie nusu kwa nusu na mkulima ili kuvutia uwekaji akiba katika nchi na kuwa na sera ya uwekezaji katika maeneo yatakayomwinua mkulima kama miundombinu ya umwagiliaji, mikopo nafuu kwa wakulima kwenye pembejeo na nyumba na bima ya afya.
  
“Nimezungumzia umuhimu wa uwazi katika matumizi ya fedha za umma ikiwemo malipo ya watumishi na viongozi wa umma. Nimewaeleza wananchi wa Nzega kuwa siku ya Jumanne kamati yangu ya Hesebu za Serikali (PAC) itaanza kukagua mahesabu ya vyama vya siasa nchini,” alisema.
  
Zitto alisema vyama vya siasa vinatumia fedha za umma takribani sh bilioni 20 kila mwaka kama ruzuku, kwamba ni haki ya wananchi kujua fedha zinatumika namna gani.
  
Alisema kuwa wananchi wa Nzega wana changamoto nyingi sana. Kwamba wakulima wa pamba walipewa madawa feki ya kuua wadudu, michango ya hovyo hovyo ni mingi mno na unyanyasi wa wana-CHADEMA ni mkubwa vijijini.

ZITTO KABWE ATAJA MSHAHARA ANAO LIPWA WAZIRI MKUU PINDA KWA MWEZI

HATIMAYE Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, ameweka wazi mshahara wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Zitto ameutaja mshahara huo wa Pinda anayejitambulisha kama ‘mtoto wa mkulima’ juzi mjini Mpanda na jana wilayani Sikonge wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika ziara ya Kanda ya Magharibi kwa ajili ya ujenzi wa chama.
Alisema Pinda anapokea jumla ya sh milioni 26, ambazo ni kiasi kikubwa kulinganisha na uchumi wa nchi.
Akichanganua alisema Pinda anapokea sh mil. 11.2 kama mbunge, sh mil. 8 kwa nafasi ya waziri na kiasi kinachosalia kufikia sh mil. 26 kwa nafasi yake ya uwaziri mkuu.
Alisema sababu hiyo ya mishahara mikubwa isiyokatwa kodi ndiyo huwafanya viongozi wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa wakali pale vyombo vya habari vinapotaka kuwafahamisha wananchi namna watumishi wao wanavyojilipa.

“Nimeanza na mshahara wa waziri mkuu pia siku zijazo nitataja na wa rais, kwa kuwa amesaini makubaliano na Serikali ya Marekani kuendesha nchi kwa uwazi, na moja ya uwazi ni kwa muajiri kujua kiasi anachomlipa mwajiriwa wake,” alisema Zitto.
Hatua ya Zitto imekuja baada ya kuwapo mvutano mkubwa kuhusiana na kile kinachodaiwa ‘usiri’ wa mishahara ya watumishi wa umma, wakati ni haki ya walipa kodi kujua kile wanachowalipa walioomba kuwaongoza.

Kodi ya laini za simu

Akizungumzia sakata la kodi katika laini za simu, Zitto alisema CCM ina ajenda ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015.

Alisema serikali baada ya kubaini watu wengi wanapeana taarifa kwa njia ya ujumbe mfupi, hususan katika masuala ya kisiasa, wakaona njia sahihi ya kudhibiti ni kuwatoza kodi ya laini ili kupunguza hatari ya mawasiliano hayo kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.

“Sikuwepo bungeni wakati wabunge wa CCM wanapitisha kadhia hiyo ya kuwanyonya wananchi, wenzangu wakaniambai tukasema hapana, kwa maana tuliona hii leo kuna Watanzania wengi wasio na uwezo wa kuhudumia simu kwa kiasi cha sh 1,000 kwa mwezi,” alisema Zitto.

Akijibu maswali ya wananchi mjini Mpanda waliotaka kujua sababu ya kupunguza makali bungeni, Zitto alisema hakuna makali yaliyopungua bali ni mitazamo ya watu.

Alisema kwa kushirikiana na wabunge wenzake wa upinzani wamekuwa wakisimamia hoja zenye manufaa kwa wananachi huku wabunge wanaojipambanua kuwa majasiri kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwaunga mkono wazi wazi.

Akiwa  wilayani Sikonge, Zitto alisema Watanzania hawawezi kujivunia uhuru huku mama zao, watoto wao na wazee wao wakiwa hawana uhakika wa kupata huduma bora ya afya, elimu na maji safi.

Alisema kwa sasa Tanzania ni taifa moja lililogawanyika katika nchi mbili za wenye fedha na wasio na fedha.


Alisema nchi ya wenye fedha, familia zao husoma katika shule bora, zenye mazingira bora na walimu wazuri, hutibiwa katika hospitali zenye hadhi na huduma muhimu na ikibidi nje ya nchi, huku nchi ya wasio na fedha  familia zao wakiishi kwa shida, kusoma katika majengo ya shule na walimu wasiopata mishahara ya kuridhisha na hospitali zisizokuwa na huduma muhimu licha ya kuchangia kiasi cha fedha kwa ajili ya bima ya afya.

UDOM YASHIDWA KUDAHILI WANAFUNZI WENGI KUTOKANA NA WANAFUNZI KUTOKUWA NA VIGEZO:

CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kimeshindwa kudahili wanafunzi wa kutosha kutokana na wahitimu kutokuwa na vigezo. Malengo ya kuanzishwa kwa chuo hicho ni kudahili wanafunzi 40,000 ifikapo mwaka 2015 lakini hadi sasa idadi ya wanafunzi waliopo hawazidi 15,000. 
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula wakati wa uzinduzi wa baraza la pili la wafanyakazi la chuo hicho.
   
Profesa Kikula alisema idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa chuoni hapo inaendelea kushuka siku hadi siku ikilinganishwa na nafasi zilizopo.

"Changamoto zinazotukabili ni nyingi lakini za msingi ni idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa imendeelea kushuka mwaka hadi mwaka kutokana na ukosefu wa wahitimu wa kutosha wenye vigezo vya kudahiliwa katika kozi zetu.

"Changamoto nyingine ni ufinyu wa bajeti unaotokana na vyanzo vichache vya mapato ya chuo na pia ufinyu wa ruzuku ya Serikali ndiyo vinakwamisha chuo kufikia malengo yake kama ilivyotarajiwa awali," alisema.

Alisema katika kukabiliana na changamoto ya kuongeza udahili, chuo kimeanzisha programu za cheti na stashahada kuanzia mwaka huu wa masomo.

Alisema kwa sasa Chuo hicho kina wanafunzi 13,376 wa shahada za awali, wanafunzi 1,403 wa shahada ya uzamili, wafanyakazi 1,181 na wataalamu 66 kutoka nje.

ZITTO KABWE AMPONDA HADHARANI PINDA NA KUDAI KUWA NI MZIGO USIOBEBEKA SERIKALINI...!!

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, amesema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ni mzigo katika serikali.
Amesema kuwa hii ni kutokana na kushindwa kufanya uamuzi mgumu katika masuala yanayolihusu taifa licha ya baadhi ya mambo kuwa katika mamlaka yake.
 
Zitto alisema kuwa hivi karibuni Pinda alishindwa kusimamia muswada wa sheria ya marekebisho ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, hali iliyosababisha kutokea vurugu bungeni.
 
Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, alitoa kauli hiyo juzi wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika kata ya Inyonga na Songambele wilayani Mlele, mkoa wa Katavi, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya kuimarisha chama Kanda ya Magharibi.
 
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona Waziri Mkuu akishindwa kukutana na kiongozi wa upinzani bungeni na kujadili masuala muhimu ya kitaifa kabla ya Bunge kuanza kwa ajili ya mustakabali wa taifa.
 
Akitolea mfano masuala kadhaa ambayo Pinda ameshindwa kuyasimamia na kumsubiri Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuyafanyia uamuzi, Zitto alitaja sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, na Yule wa Wizara ya Afya na sasa suala la kuhakikisha muafaka unapatikana katika suala muhimu la Kikatiba.
“Kama tunaye Waziri Mkuu anayekaa bungeni na kushika tama wakati nchi ikiwa katika hali ngumu ni tatizo. Huyu kila jambo anasubiri Rais atoke UN kuja kufanya uamuzi ambao yeye angeweza kuusimamia. Basi tuna kazi ya ziada katika kupata maendeleo,” alisema.
Zitto alifafanua kuwa mwanzoni alidhani Pinda anashindwa kusimamia majukumu ya serikali kutokana na kukabiliwa na jitihada za kuboresha miundombinu na maisha ya wakazi wa jimbo lake hali aliyoelezea kuwa ni tofauti na aliyoikuta.
Alisema kutokana na hali hiyo ya Pinda kutokuwa na mamlaka, wakulima wa Katavi wameendelea kununua mbolea kwa gharama ya juu licha ya serikali kutenga kiasi cha bilioni 60 kwa mwaka kwa ajili ya ruzuku ya mbolea kote nchini.
 
Alisema fedha hizo zinaliwa na wajanja huku serikali ikiendelea kuwa katika hali ya usingizi wa pono.
 
Tofauti ya CCM, CHADEMAAkizungumzia sababu ya ziara yake katika kanda hiyo, Zitto alisema ni kwa ajili ya kuhimiza mbegu ya ukombozi wa fikra na maendeleo kutoka katika mikono ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
 
Alisema wakati CHADEMA inapambana katika kila kona kuhakikisha udhalimu unaofanywa na serikali unaondoka, CCM inatumia kila njia kuhakikisha inawanyonya wananchi.
 
“Tofauti kubwa kati ya vyama hivi ni kwamba CCM inaishi kwa kuwanyonya wananchi na CHADEMA imesimama kidete kutaka udhalimu huo uondoke; na kwa ajili hiyo chama hicho tawala kinatumia kila propaganda kuhakikisha wananchi hawatuungi mkono,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, kazi ya CHADEMA siku zote imekuwa ni kuwafumbua macho wananchi juu ya unyonyaji unaofanywa na serikali ya CCM na kuwataka waepukane na propaganda za kwamba kuiunga mkono CHADEMA ni kukaribisha vita nchini.
 
Alisisitiza kuwa kwa sasa CHADEMA inajiandaa kushika dola mwaka 2015 na kwamba wanasimamia upatikanaji wa Katiba bora itakayowafanya wanasiasa kuwa watumishi wa wananachi badala ya kuwa watawala.
 
“Mmetuona kwa uchache wetu bungeni tumeweza kufanya mambo makubwa kwa nchi kila kashfa ya ufisadi mnayoisikia leo ni wabunge wa upinzani wameibua na si wa chama tawala,” alisema.
-Tanzania daima

MCHAKATO KATIBA MPYA:JK: Hoja ya Z`bar irudishwe bungeni

*Apinga maandamano ya wapinzani
*Awakaribisha Ikulu kwa majadiliano
*Amshushua Tundu Lissu, asema mzushi
*Kuvunjwa Tume ya Warioba afafanua
Rais Jakaya Kikwete, amekata mzizi wa fitina katika suala la mchakato wa katiba kwa kushauri ile hoja ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria  na Utawala kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar, ilirudishwe Bungeni ili wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka.
Aidha, amevitaka vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kuachana na mipango ya maandamano na kufanya ghasia kama dhamira yetu ni kutaka kupata Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba na Sheria.
Kauli hiyo ya Rais imekuja kukiwa kumebakia siku tano zilizotangazwa na viongozi wakuu wa vyama hivyo kwa ajili ya kufanya maandamano nchi nzima kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa wakati wa mkutano wa 12 wa Bunge mwezi uliopita.

 Rais Kikwete alisema aliambiwa kuwa kuliwepo madai ya Zanzibar kutokushirikishwa ipasavyo katika kutoa maoni kwenye muswada huo.
“Nimeeleza kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika Muswada.  Hivyo basi napata tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa msingi wake nini!  Labda kuna kitu sikuambiwa,”alisema
Hoja kwamba Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar, aliambiwa kuwa kanuni za Bunge hazina sharti hilo, hivyo kamati haistahili kulaumiwa.
Rais Kikwete alishauri kama ni hivyo, suala hilo lirudishwe Bungeni ili wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka, vinginevyo watu wataendelea kulaumiana isivyostahili. 

Alisema, “kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la kukataa Muswada au kususia vikao vya Bunge au kufanya maandamano sidhani kama ni sawa”. 

MAANDAMANO YA WAPINZANI
Rais Kikwete alisema kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama Mwenyekiti wa Chadema, freeman Mbowe anavyotaka hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hii.
“Kuna msemo wa wahenga kuwa “historia hujirudia”.  Naomba hekima ziwaongoze viongozi wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia mwaka 2012,”alisema.
Alisema kuwa mwaka jana, kulipotokea mazingira ya kutoelewana katika suala la katiba, pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na  baada ya kuridhiana hatua zipasavyo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo.

Alisema kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu na badala yake tutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima na kwamba tukikataa kufanya hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu.
 “Watanzania watakuwa na haki ya kuuliza nia ni hii yetu sote ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria au tuna dhamira nyingine iliyojifisha?, alihoji Rais Kikwete.

Alisema viongozi wa vyama hivyo watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na kisheria kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa kuboresha  Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kufanya hivyo kutasaidia  kujenga Taifa badala ya kubomoa.
Aliongeza kuwa baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani zimemsikitisha sana na madai na tuhuma za uongo kwamba katika uteuzi wa Tume ya Katiba hakuheshimu mapendekezo ya Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Baraza la Kikristo (CCT) na walemavu.
AMSHUSHUA LISSU
“Siyo tu kauli hiyo ya Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki) ni uzushi na uongo mtupu bali pia ni ya unafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu.  Nasema hivyo kwa sababu, sipendi kuamini kuwa mbunge amesema yale kwa kutokufahamu ukweli au kwa bahati mbaya.”
Rais alisema mbunge huyo aliamua kupotosha ukweli ili pengine isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wajumbe 166 wa Bunge Maalum la Katiba.
Alisema hashabikii jukumu hilo, lakini kwa kutimiza wajibu na maslahi ya taifa akiagizwa na sheria za nchi atalifanya.

Akilinganisha na uteuzi wa wajumbe 30 wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Rais Kikwete alisema haikuwa rahisi hata kidogo na hii ya uteuzi wa watu 166 watakaoingia katika Bunge Maalum la Katiba itakuwa ngumu zaidi.
Alieleza kuwa licha ya kutakiwa kuteua watu 30 wajumbe walioteuliwa na wadau walikuwa zaidi ya 500  akieleza kuwa kwa Zanzibar zilikuwa asasi zaidi ya  60  wakati Bara  zilikuwa asasi zaidi ya 170 zikiwa na waombaji zaidi ya 500.
Alisema uteuzi ulihakikisha kuwa wawakilishi wa  vyama vya siasa vyenye wabunge na wajumbe Baraza la Wawakilishi wanapatikana,  mashirika ya dini kubwa ya  TEC, CCT na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata)  pia wanakuwepo.
Alisema kwa upande mwingine Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ilipendekeza uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar.  Pia SMZ ilishauri kwamba kama Bunge Maalum litashindwa kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa, liongezewa muda hadi kufikia siku 90.
“Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa kuwateua wajumbe wa Bunge Maalum.”
Alisema dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu ingefaa kama kungekuwepo na nafasi za kutosha kwa  kila kundi nchini.  Rais alisema pendekezo hilo haliwezekani, labda kuwe na Bunge Maalum lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.
MUSWADA BUNGENI
Rais Kikwete aliwaambia wapinzani kuwa  mapendekezo yao kuhusu marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba hayawezi kuzungumzwa nje ya Bunge.
Alisema maoni yao yangezungumzika na hata baadhi yangekubalika kama wasingetoka nje wakati wa mjadala huo uliozua tafrani bungeni mwezi uliopita.
Aliongeza kuwa baada ya wapinzani kupoteza fursa halali kutoa mapendekezo yao na sasa kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana.
“ Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni na si vinginevyo,”alisema.
Aliwaambia kuwa kwa vile hawakuwepo ndani ya mjadala na  hakuna aliyewawakilisha hivyo hakuna kinachoweza kufanyika.

WAJUMBE BUNGE LA KATIBA
Rais Kikwete alisema kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema sababu ya idadi ya wajumbe wa tume kuwa sawa inatokana na utaratibu wao wa kufikia uamuzi, kwani ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga kura.
Alifafanua kuwa, Bunge maalum la Katiba lina sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya kura za kila upande kukubali, bila ya hivyo hakuna uamuzi, hivyo katika bunge hilo nguvu si uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza kupata bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila upande peke yake.

“Zanzibar ina majimbo 50 ya uchaguzi na Tanzania Bara ina majimbo 189, hivyo ukiamua kwa wingi kila wakati Wazanzibari watashindwa.  Lakini, hapajakuwepo madai ya Zanzibar nao kutaka kuwa na idadi sawa ya majimbo kama Bara au kupunguza majimbo ya Bara yawe sawa na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja,”alisema.

Alisema msingi unaotumika ni kutoa nguvu sawa za uamuzi kwa kila upande wa Muungano wakati wa kuamua masuala ya Katiba, hakuna mdogo wa kumezwa na mkubwa, wote wako sawa.

 KUVUNJWA TUME YA WARIOBA

Alisema kumekuwepo na madai ya wapinzani kuhusu suala la uhai wa Tume ya Katiba ambao wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalum bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato.

Aliongeza kuwa  suala la ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba siyo mapendekezo ya Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala bali lilitokana na pendekezo la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na wabunge wengi.
 “Nami naiona hoja ya wajumbe wa tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume.  Je ushiriki huo uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo linaloweza kujadiliwa,”alisema.
Jumanne wiki hii, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, akizungumzia suala la ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema suala hilo lilipendekezwa na Mbunge wa Kisarawe, Suleman Jaffer.
Chikawe alisema mbunge huyo alipendekeza kuwa tume hiyo itakapowasilisha ripoti yake ivunjwe sababu haitakuwa na kazi na kama Bunge la Katiba litahitaji ufafanuzi wowote ataitwa Mwenyekiti wa Tume hiyo kutoa ufafanuzi.


MUSWADA KUHODHIWA NA CCM

Chikawe alisema kama unachukua Bunge kwa misingi ya chama siyo sawa lakini bunge halikukutana na kupitisha muswada huo kwa misingi hiyo.

“Kitu cha msingi ni kwamba kolamu ya wabunge ilitimia wakati wa kupitisha muswada huo, hivyo sheria haikuvunjwa,sikuona sababu ya wabunge wa upinzani kutoka Bungeni,”alisema.

Alisema tabia ya wabunge wa vyama vya upinzani kutoka bungeni na kukimbilia mitaani na kwenda kuwapotosha wananchi siyo sahihi.

KUMTISHA RAIS ASIPOSAINI MUSWADA

Alisema yeye (Chikawe) hana ubavu wa kumtisha Rais kwani Rais ana hiari ya kuusaini muswada huo au kutousaini.
“Ni imani yangu kwamba Rais atasaini muswadam atatumia ustaarabu wake,”alisema Chikawe.

Juzi viongoz wa Kamati ya Ufundi ya Ushirikiano wa Vyama vya CUF,Chadema na NCCR-Mageuzi walisema maandalizi kwa ajili ya maandamano hayo yatakayofanyika Oktoba 10 mwaka huu, yameanza kufanyika baada ya kuwasiliana na viongozi wa mikoa yote.

SHAMBULIZI LA KIGAIDI NAIROBI

Rais Kikwete alisema tangu shambulio lililotokea mwaka 1998, Serikali imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi katika nyanja mbalimbali.

”Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku hadi siku.  JWTZ, Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo.  Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa,”alisema.

Rais Kikwete alisema baada ya tukio la Kenya, vyombo vya ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu na kwamba pamoja na kujizatiti kwetu huko hatuwezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini.

Alisema uhakika huo haupo kwani hata mataifa makubwa na tajiri yameshambuliwa, hivyo jambo la muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na wananchi kusaidia ili  vyombo vya ulinzi na usalama  vifanikiwe zaidi. 
 
Aliongeza kuwa watu wote wenye shughuli zinazokusanya watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa waweke kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo yao na kuweka vifaa vya upekuzi (metal detectors and x-rays). 

Rais Kikwete alisema wananchi waendelee kufanya shughuli zao bila ya hofu ingawaje wasiache kuwa makini na kuchukua tahadhari, na kwamba maafisa husika wa vyombo vya ulinzi na usalama wataendelea kuelimisha umma kuhusu hatua mbalimbali za tahadhari za kuchukua. 

HII NDIO MIKOA YA TANZANIA INAYOSADIKIKA KUWA NA UTAJIRI MWINGI,BOT


Kwa mujibu  wa ripoti ya Benki kuu ya Tanzania(BOT),Dsm ndio mkoa unaoongoza kwa kuchangia pato la taifa. 

1. Dar-es-salaam(GDP-7.5 trilion)
2. Mwanza(GDP-4.09 trilion)
3. Mbeya(GDP-3.2 trilion)
4. Shinyanga
5. Iringa
6. Morogoro
7. Arusha(GDP-2.1 triliom)
8. Tanga(GDP-2.09 trillion)
9. Kilimanjaro(GDP-2.03 trillion)

Cha kushangaza ni kuwa mkoa wa Lindi ambao umezungukwa na gesi yenye ujazo wa mabilioni ndio mkoa wa pili kwa umaskini baada ya mkoa wa Pwani.
Lakini swali ni je,kwanini arusha haipo hata katika top 3 ya mikoa tajiri yenye kuchangia pato la taifa? Inaonekana makampuni mengi ya utalii yanamilikiwa na wageni au mengi yanatokea katika mkoa wa Dsm.