Muigizaji wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ amekataa kabisa suala la
kuolewa kwa sasa akidai moyo wake haupo tayari kwa tendo hilo.
Lulu
alifunguka hayo Jumatatu iliyopita katika kipindi cha Mkasi
kinachorushwa kupitia Runinga ya East Africa ambacho humpa nafasi staa
kuzungumzia mambo mbalimbali yanayohusu maisha yake na sanaa kwa jumla.
Wakati
mahojiano hayo yakiendelea, mmoja wa watangazaji wa kipindi hicho
anayefahamika kwa jina la Muba, alimtupia Lulu swali ambalo lilimtaka
aeleze utayari wake endapo mtu akijitokeza na kutaka kumuoa.
“Sitaki
kuolewa kwa sasa, muda wa kuolewa haujafikia. Ukifika nitafanya hivyo
lakini kwa sasa sipo tayari kuolewa,” alisema Lulu.
Aidha,
Lulu alikiri kuwa licha ya kutokuwa tayari kuolewa lakini amekuwa
akipata usumbufu mkubwa wa kutongozwa na wanaume. Aliainisha kuwa
alikuwa akitongozwa kabla na baada ya kutoka Segerea alipokuwa
akishikiliwa kwa kesi ya kifo cha aliyekuwa mpenzi wake, marehemu Steven
Kanumba.
“Watu wananitongoza sana, walikuwa wakifanya hivyo kabla hata
sijaingia China (gerezani Segerea) na wameendelea kufanya hivyo hata
baada ya kutoka,” alisema Lulu na kuongeza:
“Siwezi kuwakubalia sababu sipo tayari kuolewa kwa sasa…muda wa kufanya hivyo haujafika.”
Kuhusu
suala la kudaiwa kutembea na bosi wa Kampuni ya Proin Promotion ambayo
inamsimamia kisanii kwa sasa, Lulu aliruka viunzi na kudai taasisi hiyo
inamlea kama mtoto wa familia na siyo vinginevyo.
Alisema hata madai
yanayoelekezwa kwake kuwa Proin wamempa gari na nyumba kama sehemu ya
kuhongwa na bosi wa kampuni hiyo, hayana ukweli wowote kwani yeye
anafanya kazi kama msanii chini ya kampuni hiyo na hakuna kitu cha
ziada.
“Hahahaha! Salama (mtangazaji) acha mambo yako bwana… mimi
nipo chini ya Proin kwa sasa kwa kipindi flani ambacho nimesaini nao
mkataba. Wananilea kama msanii wao, hakuna cha ziada,” alisema Lulu.
Akiendelea
kubwabwaja maneno ndani ya kipindi hicho, Lulu aliweka wazi kuwa
alikuwa akishindwa kuanika penzi lake na marehemu Kanumba kwa kuwa muda
muafaka ulikuwa haujafika na kudai waliishi kama mtu na baba yake kabla
hawajawa wapenzi, wakawa wapenzi na mauti yakamkuta Kanumba kabla
hawajalianika penzi lao.