Wewe ni rapper unayetumia Kiswahili na Kiingereza kufanya muziki wako? Style hii imepewa jina ‘Swaghili’ na rapper Gosby ambaye yeye na Wakazi kwangu mimi ni mfano wa kuigwa na rappers wengine wa aina yao. Haya ni mambo 10 ya kuiga kutoka kwao
1. Kujielewa na Kuwaelewa Walengwa wa muziki wao
Hii ni sababu kubwa ambayo rappers wengine wa aina ya Gosby na Wakazi wanashindwa kuizingatia. Unapofanya muziki wa aina hii, maana yake ni kuwa, muziki wako una wigo mpana zaidi nje ya Tanzania. Ukijielewa hivyo, hutakuwa unapita njia kama anazoweza kuzipitia Juma Nature kupromote nyimbo zake. Gosby kwa mfano: Anajielewa kuwa muziki wake ni wa aina fulani ya vijana wa leo, wanaojua Kiingereza, wameenda shule kiasi na wasomi pia, wasichana (hususan masista du) na nyimbo anazotoa nyingi zinahusu maisha yao. Ni rahisi kurelate nao kwasababu kama akiimba mapenzi, basi anaimba yale yanayowazunguka wao. Na ndio maana, pamoja na kwamba muziki wa aina yake Kibongobongo unaonekana kama haulipi, Gosby amejikusanyia mashabiki wengi mno wa kike ambao husikiliza nyimbo zake.
Rappers wengi wa aina yake, hawawaelewi walengwa wa nyimbo zao na hawajui namna ya kuwafikia.
2. Uvumilivu na Unyenyekevu
Katika mazungumzo yangu hivi karibuni na Gosby, alinisimulia jinsi producer Dunga alivyomsumbua kurekodi wimbo wake licha ya kuwa amemlipa pesa yake. Aliniambia kuwa Dunga alimzungusha kwa zaidi ya wiki moja ambapo kila siku alikuwa akimpiga tarehe ‘njoo kesho’. Alisema hatimaye siku moja alimsurprise na kurekodi wimbo wake na siku hiyo hiyo kumaliza kila kitu na kumkabidhi CD yake. Dunga alimueleza kuwa alitaka kumfundisha umuhimu wa kuwa mvumilivu na mnyenyekevu. Ukiwa mvumilivu na kujishusha hata katika mazingira magumu kabisa, ni rahisi kufanikiwa na kupendwa.
3. Ubishi
Wakazi aka The Bilingual Beast ana fundisho la muhimu sana kwa wasanii wachanga katika muktadha huu. Aliwahi kunisimulia jinsi ilivyokuwa ngumu kwake kupromote mixtape zake tatu nchini. Ilikuwa ngumu wabongo kumwelewa mara moja hasa kwakuwa alikuwa nchini Marekani. Alisema alikuwa hachoki kuzitumia blogs nyingi za Bongo nyimbo za mixtape yake lakini zingine zilipuuza. Hilo lilimfanya aamue kufungua blog yake mwenyewe kibishi na kuanza kuandika mambo yake. Alisema alishangaa jinsi ilivyopata mashabiki na watu wengine waliokuwa wakipuuza kuanza kutumia kile alichokiweka.
4. Kutokata tamaa
Kama Wakazi angekataa tamaa baada ya kuona watu wamezichukulia poa mixtape zake tatu za ‘Mixtape Ya Ukweli’, angekuwa ameshaacha muziki siku nyingi. Lakini ameendelea kukomaa hadi sasa watu wameshamuelewa.
5. Kujituma
Wakati Gosby anasambaza CD za wimbo wake mpya, Monifere aliowashirikisha Vanessa Mdee na Jux, hakuona tabu kuzunguka mitaa mingi ya jiji la Dar es Salaam kuwagawia CD wadau muhimu tofauti kabisa na vyombo habari wakiwemo mashabiki wake pia. Kwa msanii mwingine, hiki si kitu rahisi kufanya.
Wakazi pia anajulikana kwa moyo wake wa kujituma, na ndio maana mwaka huu alipata shavu la kwenda kutumbuiza kwenye eviction show ya Big Brother Africa.
6. Kutafuta fursa mtandaoni
Hapa ndipo rappers wengi wa aina ya Wakazi na Gosby huchemka. Mfano mzuri ni jinsi Gosby alivyofanikiwa kuingiza wimbo wake BMS kwenye mixtape maarufu duniani ya Coast 2 Coast na jinsi ambavyo mashairi ya nyimbo zake yamekuwa yakiwekwa kwenye mtandao mkubwa duniani wa rapgenius.com. Hakuna anayemshika mkono kufanya hivi, ni yeye mwenyewe. Kwa namna ambayo Gosby anatumia fursa vizuri za mtandaoni, ni rahisi sana kupata connections kubwa za kimataifa zikiwemo kuonwa na record label kubwa na kumchukua siku moja.
Kwa upande wa Wakazi, mwaka juzi producer wa Nigeria, Don Jazzy, aliweka shindano la kutafuta rapper Afrika ambaye angeitumia vizuri beat yake aliyoipa jina, Enigma. Wakazi naye alijaribu bahati yake na kutuma verse yake. Japo hakushinda, lakini uwezo aliounesha kwenye beat hiyo ulimuongezea wigo barani Afrika.
7. Kutumia vizuri mitandao ya kijamii
Ingia kwenye ukurasa wa Twitter wa Gosby na utaona jinsi anavyointerect na mashabiki, washkaji na wadau muhimu. Jana #Monifere ilikuwa inatrend kwenye Twitter nchini. Rappers kama Cyrill na Cliff Mitindo wanapaswa kuiga mfano huu.
Wakazi pia ni bingwa wa kutumia vyema mitandao hii. Mara nyingi amekuwa akiitumia Twitter kuwakumbusha mashabiki wake kuomba nyimbo zake kwenye vituo vya radio.
8. Ubunifu
Unakumbuka jinsi Gosby alivyowaalika wasichana watatu kwenye kwenye listening session ya wimbo wake BMS? Huo ni ubunifu mkubwa. Juzi alitoa ofa ya CD ya bure ya wimbo wake Monifere kwa shabiki yeyote ambaye angebadilisha picha ya profile ya Facebook au Twitter na kuweka cover la Monifere, huo ni ubunifu.
9. Kubadilika ‘Versatility’
Nani alitegemea Gosby angefanya wimbo kama BMS ama Monifere? Nani alitegemea Wakazi anaweza kurap kwenye beat ya house za Afrika Kusini?
10. Simplicity
Hii ndio silaha kubwa zaidi ambayo rappers wengine wa aina ya Wakazi na Gosby hawana. Kuwa simple, kutokuwa na dharau kuheshimu kila kitu na kuwa mtu wa watu.